Leo tarehe 24 Aprili 2025, Mhe. Caesar C. Waitara, Balozi wa Tanzania nchini Namibia amekutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Ubalozi na baadhi ya watoa mada katika Kongamano linalohusu mchango wa Lugha ya Kiswahili katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika hususan Namibia. Kongamano hilo litafanyika tarehe 25 Aprili 2025 jijini Windhoek.

Watoa mada hao waliofika Ubalozini ni Balozi Lt.Gen.(Rtd) Abdulahrahman Shimbo, aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Balozi wa Tanzania nchini China pamoja na Balozi Brig.Gen.(Rtd) Francis Mndolwa, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Balozi wa Tanzania nchini Burundi.

Aidha, watoa mada wengine kutoka Tanzania ambao watakuwepo katika Kongamano hilo ni Bi. Consolata Mushi, Katibu Mtendaji wa BAKITA ambaye anamwakilisha Mhe. Prof. Aidan Mwaluko Kabudi (MP), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Eliah Victor, Mkurugenzi wa Vipindi wa TBC ambaye anamwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TBC.