Leo tarehe 2 Juni 2026, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia umefanya hafla fupi ya makabidhiano rasmi ya mfumo wa usimamizi wa maktaba wa KOHA uliosimikwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Namibia (UNAM).
Utekelezaji na uanzishwaji wa mfumo huu umefanyika kupitia ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia na Chuo Kikuu cha Namibia ( UNAM), ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha huduma za maktaba ya Kiswahili ya Ubalozi pamoja na mifumo yake ya usimamizi.
Mfumo huu utaboresha usimamizi wa rasilimali za maktaba, kurahisisha upangaji na uorodheshaji wa vitabu, pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watumiaji wa Maktaba ya Kiswahili ya Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia. Aidha, utachangia katika kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili, kuongeza upatikanaji wa maarifa, na kuimarisha ushawishi wa Kiswahili ndani ya Namibia na nje ya mipaka yake.
Muhimu zaidi, mfumo huu wa KOHA ni wa kwanza kutumika katika Maktaba ya Kiswahili ndani ya Balozi za Tanzania nje ya nchi. Hivyo, utachukuliwa kama mradi wa majaribio (pilot project) na mfano wa kuigwa, ambao utaweza kupanuliwa na kutumika katika balozi nyingine za Tanzania duniani.
Hatua hii ni sehemu muhimu ya juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuimarisha mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa maktaba, pamoja na kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa.







