Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia ulishiriki katika maonyesho yaliyofanyika sambamba na Mkutano wa Afrika wa Biashara na Uwekezaji wa mwaka 2026 uliofanyika mjini Swakopmund, Namibia mwishoni mwa mwezi Mei 2026.
Kupitia maonyesho hayo, Ubalozi ulipata fursa ya kuonesha bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini. Aidha, Ubalozi ulihamasisha wawekezaji kutoka Namibia na nchi nyingine zilizoshiriki mkutano huo kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zenye uwezo mkubwa wa ukuaji na kuleta tija kiuchumi.
Sekta zilizotangazwa ni pamoja na mifugo, utalii, viwanda na uchakataji wa mazao, uchumi wa buluu, nishati, pamoja na madini. Maonyesho hayo pia yalitoa fursa muhimu ya kujenga na kuimarisha mitandao ya kibiashara na uwekezaji (networking) kati ya washiriki kutoka nchi mbalimbali za Africa, na hivyo kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi.
Ushiriki wa Ubalozi katika maonyesho hayo ulikuwa sehemu ya utekelezaji wa kidiplomasia ya uchumi inayolenga kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania, Namibia na nchi nyingine za Afrika.







