Tarehe 01 Juni 2026, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia ulipokea ujumbe wa Wataalamu kutoka mamlaka mbalimbali za maji nchini Tanzania waliowasili nchini Namibia kwa ziara ya siku tano ya mafunzo na kubadilishana uzoefu kuhusu utoaji wa huduma za maji na uendeshaji wa mamlaka za maji kwa misingi ya kibiashara. Ujumbe huo unaongozwa na Bw. Prosper Buchafwe, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Maji ya Tanzania.

Ziara hiyo inalenga kuwawezesha wataalamu hao kujifunza mbinu, mifumo  na uzoefu mbalimbali unaotumika katika kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira, kuongeza mapato ya mamlaka za maji, pamoja na kupunguza utegemezi wa ruzuku za Serikali katika kugharamia shughuli za uendeshaji.