Balozi wa Tanzania nchini Namibia Mhe. Caesar C. Waitara, amefungua mafunzo maalum ya lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya awali jijini Windhoek, Namibia.

Akifungua mafunzo hayo Julai 25, 2025 Balozi Waitara ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya ufunguzi huo, ameeleza kuwa mafunzo hayo ni matokeo ya Kongamano la Kwanza la Kiswahili lililoandaliwa na Ubalozi mwezi Aprili 2025 ambalo lilifanyika katika Chuo cha Triumphant.

Mafunzo hayo yatakayofanyika katika kipindi cha wiki 15, yatatolewa kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 29 Julai 2025, katika Chuo cha Triumphant kilichopo Windhoek, Namibia kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA).

Aidha, katika hotuba yake, Mhe. Balozi Waitara aliwapongeza wanafunzi wa chuo hicho kwa kuamua kujifunza lugha hiyo kwa sababu pamoja na masuala mengine, itawezesha kuwasiliana kirahisi na raia zaidi ya milioni 200 wa mataifa mengine ambao wanazungumza lugha hiyo muhimu.

Hadi hivi sasa idadi ya wanafunzi ambao wameshajiandikisha kwa ajili ya mafunzo hayo ni 70 wakiwemo Balozi wa Namibia nchini Nigeria, Balozi wa Namibia nchini Jamhuri ya Watu wa Congo pamoja na Konseli Mkuu wa Namibia aliyopo Angola.

Balozi Waitara aliendelea kuwasisitiza wanafunzi hao kuhusu umuhimu wa lugha hiyo kama utambulisho wa Mwafrika, kuleta umoja na kusaidia katika mawasiliano na uendeshaji wa biashara.

Vilevile, lugha hiyo itaongeza wigo wa uelewa wa wanafunzi katika masuala mbalimbali ikiwemo biashara, utamaduni, utalii na diplomasia.

Mbali na hayo Mhe. Balozi Waitara aliahidi kuwa  Ubalozi wa Tanzania utaendelea kushirikiana na Triumphant College, BAKITA, na wadau wengine katika kuimarisha lugha ya Kiswahili nchini Namibia. 

Tukio hilo lilifanyika kwa njia ya Hybrid ambapo kwa upande wa Namibia lilihudhuriwa na Prof Geoffrey Kiangi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Triumphant, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia pamoja na wanafunzi wa Kiswahili.

Kwa njia ya mtandao, tukio hilo lilihudhuriwa na Waheshimiwa Mabalozi wa Namibia wanaowakilisha Namibia nchini Nigeria pamoja na Jamhuri  ya Watu wa Congo pamoja na Bi. Consolata Mushi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania.