Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia umeshiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Ongwediva (Ongwediva Annual Trade Fair - OATF) yaliyofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 31 Agosti 2025, katika mkoa wa Oshana nchini Namibia).

Maonesho hayo ya kila mwaka huwakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kuonesha na kutangaza bidhaa na huduma kutoka katika nchi zao. Ubalozi wa Tanzania umekuwa mshiriki wa kudumu katika maonesho haya kama sehemu ya mkakati wa kidiplomasia wa kiuchumi kwa ajili ya kutangaza bidhaa, huduma, pamoja na fursa za uwekezaji na biashara zinazopatikana nchini Tanzania.

Maonesho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 24 Agosti 2025 na Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi Ndaitwah, Rais wa Namibia, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri  mkuu na Waziri wa Viwanda, Madini na Nishati wa Namibia, pamoja na mawaziri wengine wa serikali ya Namibia, wakuu wa mikoa, wabunge, na mabalozi kutoka nchi mbalimbali.

Kwa mwaka huu, Tanzania iliwakilishwa na wajasiliamali mbalimbali waliowasilisha bidhaa mbalimbali za asili ya Tanzania. Aidha, Watanzania waishio Namibia (Diaspora) walishiriki kikamilifu kwa kuuza bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania, hali iliyoonesha mshikamano mzuri baina ya Ubalozi na Diaspora.

Ubalozi wa Tanznia uliandaa banda maalum lililotumika kutangaza bidhaa mbalimbali za Kitanzania ikiwemo mchele, maharage, kahawa, chai, korosho, mvinyo, konyagi, pamoja na viungo kutoka Zanzibar. Moja ya vivutio vya kipekee mwaka huu lilikuwa ni maandazi na chakula cha jadi cha wali na maharage, ambacho kilipokelewa kwa furaha kubwa na wageni waliotembelea banda hilo.

Mwitikio kutoka kwa wanachi wa Namibia ulikuwa mkubwa, ambapo wafanyabiashara na wateja binafsi walionesha nia ya dhati ya kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na watengenezaji wa bidhaa kutoka Tanzania. Baadhi yao waliunganishwa moja kwa moja na mfanyabiashara Mtanzania anayeendesha shughuli zake mjini Windhoek, ambaye husambaza bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania.

Ubalozi unaamini kuwa ushiriki wa mwaka huu umeendelea kuimarisha jina la Tanzania katika soko la Namibia na Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ujumla, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza mahitaji ya bidhaa za Kitanzania. Hii ni hatua muhimu katika kuendeleza mahusiano ya kiuchumi, kibiashara na kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia.