Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia ulishiriki katika Maonesho ya Mwaka ya Biashara ya Ongwediva (OATF) yaliyofanyika kuanzia tarehe 26 Agosti hadi 01 Septemba 2022. Haya ni maonesho yaliyowazi kwa wajasiriamali wa ndani, kikanda na kimataifa, wafanyabiashara na mashirika.
OATF iliyofanyika chini ya kaulimbiu “Kujenga Uchumi Bora” ilifunguliwa rasmi na Mheshimiwa Nangolo Mbumba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Namibia kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Hage G. Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia mnamo tarehe 28 Agosti 2022. Ufunguzi huo ulihudhuriwa na Mh. Saara Kuugongelwa Amadhila, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Namibia.
Katika kuendeleza diplomasia ya Uchumi, Ubalozi ulitumia fursa hii kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuonesha na kuuza bidhaa za Kitanzania, kutafuta masoko mapya na kupata fursa mpya. Bidhaa hizo zilijumuisha vyakula (maharage), vinywaji (mvinyo na konyagi), mavazi ya Kitanzania (mashati na magauni ya vitenge, vikoi, shanga, bangili, mikoba na vikapu), mapambo ya kiutamaduni, korosho, kahawa, viungo vya chai, majani ya chai pamoja na vitabu ya Kiswahili.
Ubalozi ulipata fursa ya kutembelewa na wageni mbalimbali, hususan wale ambao walipata hifadhi Tanzania kipindi cha miaka ya kugombania uhuru. Hata hivyo ubalozi ulichukua mawasiliano yao kwa kumbukumbu.